Ushairi ni utungo wa kisanaa unaotumia lugha teule na mpangilio fulani wa maneno badala ya kutumia lugha natharia(mflulizo).
Ushairi unaweza kuwa kipera cha fasihi simulizi (nyimbo) na pia katika fasihi andishi kwa sababu mashairi yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya kukariri na pia kwa njia ya maandishi. Mashairi yanayoghanwa badala ya kuimbwa huitwa maghani.
Uchambuzi
Katika ushairi, tutaangalia:- Aina za Mashairi - Kuainisha mashairi kulingana na idadi ya mishororo katika kila ubeti.
- Bahari za Ushairi - Muundo wa shairi kulingana vina, idadi ya mizani, vipande, mpangilio wa maneno n.k.
- Uchambuzi wa Mashairi - Mambo muhimu unayohitajika kuzingatia unapochambua shairi
- Uhuru wa Mshairi - Ukiukaji wa kanuni za sarufi
- Istilahi za Kishairi - Msamiati unaotumika katika ushairi km vina, mizani n.k
- Sifa za Ushairi - Sifa zinazobainisha ushairi kutokana na aina nyingine za sanaa.
- Umuhimu wa Ushairi - Umuhimu wa ushairi katika jamii.
Istilahi za Kishairi
Haya ni baadhi ya maneno ambayo hautakosa kukutana nayo unapozingatia ushairi. Ni muhimu mwanafunzi kuyajua vizuri.- Shairi - ni sanaa ya maneno (utunzi maalum wa lugha ya kisanaa) unaotumia mpangilio na uteuzi maalum wa maneno na sauti ili kupitisha ujumbe fulani.
- Vina - ni silabi za mwisho katika kila kipande.
- Mizani - ni idadi ya silabi katika kila mshororo.
- Mshororo - ni msitari mmoja wa maneno katika shairi.
- Ubeti - ni kifungu cha mishororo kadhaa.
- Vipande - ni visehemu vya mshororo vilivyogawanywa kwa alama ya kituo(,)
- Ukwapi- kipande cha kwanza katika mshororo
- Mwandamo - Kipande cha tatu katika mshororo
- Ukingo - kipande cha nne katika mshororo
- Utao - kipande cha pili katika mshororo
- Mwanzo - mshororo wa kwanza katika ubeti
- Mloto - mshororo wa pili katika ubeti
- Kimalizio/Kiishio - mshororo wa mwisho katika ubeti usiorudiwarudiwa katika kila ubeti.
- Kibwagizo - mshororo wa mwisho katika ubeti unaorudiwarudiwa kila ubeti.
Sifa za Ushairi
- Huwa na vina, mizani, mishororo na beti
- Hutumia lugha teule
- Hufupisha au kurefusha maneno ili kutosheleza idadi ya mizani
- Mashairi hayazingatii kanuni za kisarufi. (Angalia uhuru wa mshairi)
- Hutumia mbinu za lugha
Umuhimu wa Mashairi
- Kuburudisha
- Kuhamasisha jamii
- Kukuza sanaa na ukwasi wa lugha
- Kuliwaza
- Kuelimisha
- Kuonya, kutahadharisha, kunasihi na kuelekeza
- Kupitisha ujumbe fulani
- Kusifia mtu au kitu
- Kukejeli au kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya jamii
Aina za Mashairi
Shairi moja haliwezi kuwa la aina mbili (k.v tarbia na takhmisa) lakini shairi linaweza kuwa katika bahari zaidi ya moja.
Zifuatazo ni aina za mashairi kulingana na idadi ya mishororo katika kila ubeti
AINA | MISHORORO | |
Umoja/tathmina | 1 | Tathmina au Umoja ni shairi lenye mshororo mmoja katika kila ubeti. |
Tathnia | 2 | Tathnia ni shairi lenye mishororo miwili katika kila ubeti. |
Tathlitha | 3 | Tathlitha ni shairi lenye mishororo mitatu katika kila ubeti. |
Tarbia | 4 | Tarbia ni shairi lenye mishororo minne katika kila ubeti. Mashairi mengi ni ya aina ya tarbia. |
Takhmisa | 5 | Takhmisa ni shairi lenye mishororo mitano katika kila ubeti. |
Tasdisa | 6 | Tasdisa ni shairi lenye mishororo sita katika kila ubeti. |
Usaba | 7 | Usaba ni shairi lenye mishororo saba katika kila ubeti. |
Ukumi | 10 | Ukumi ni shairi lenye mishororo kumi katika kila ubeti. |
Bahari za Ushairi
Mifano ya Bahari za Ushairi
- Utenzi - shairi ndefu lenye kipande kimoja katika kila mshororo.
- Mathnawi - ni shairi la vipande viwili (ukwapi na utao) katika kila mshororo.
- Ukawafi - ni shairi la vipande vitatu (ukwapi, utao na mwandamo) katika kila mshororo.
- Mavue - Shairi la vipande vinne (ukwapi, utao, mwandamo na ukingo) katika kila mshororo.
- Ukaraguni - shairi ambalo vina vyake vya kati na vya mwisho hubadilika kutoka ubetio mmoja hadi mwingine.
- Ukara - shairi ambalo vina vya kipande kimoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya kipande kingine hubadilika. Kwa mfano, vina vya kati vinafanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho lakini vina vya kipande cha mwisho vinabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
- Mtiririko - shairi ambalo vina vyake vya mwisho na vya kati havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.
- Mkufu/pindu - Shairi ambalo neno la mwisho au kifungu cha mwisho cha maneno katika ubeti mmoja, hutangulia katika ubeti unaofuatia.
- Kikwamba - Neno moja au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa kutanguliza mishororo au ubeti katika shairi.
- Kikai - Shairi lenye kipande kimoja kifupi (chenye mizani chache kuliko kingine) Mfano (8,4)
- Msuko - Shairi ambalo kibwagizo/mshororo wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo mingineyo. K.v (8,8) (8,8) (8,8) (8).
- Mandhuma - shairi ambalo kipande kimoja hutoa hoja, wazo ama swali, huku cha pili kikitoa jibu/suluhisho.
- Malumbano - Mashairi mawili ambapo mshairi mmoja hutunga shairi akijibu au kupinga utunzi wa mshairi mwengine.
- Ngonjera - Shairi lenye wahusika wawili wanaojibizana. K.m. Ubeti wa kwanza, mwalimu, na wa pili, mwanafunzi.
- Sakarani - Shairi lenye bahari zaidi ya moja.
- Sabilia - Shairi lisilokuwa na kibwagizo. Kituo (mshororo wa mwisho) hubadilika kutoka ubeti hadi ubeti.
- Shairi huru - shairi lisilozingatia sheria za ushairi
- Shairi guni - shairi lenye makosa ya arudhi za shairi
'' Ewe mtunga silabi, na sauti ya kinubi,
Majukumu hatubebi, maadamu hatushibi,
Mateso kwa ajinabi, kwa mabwana na mabibi
Ukija hayatukabi, karibia karibia ''
'' Nashindwa nikupe nini, nishukuru kwa malezi, mapenzi na riziki,
Ni pendo kiasi gani, lishindalo la mzazi, kweli mama hulipiki,
Ulinilinda tumboni, ukilemewa na kazi, ila moyo huvunjiki,
Kanilisha utotoni, mavazi pia malazi, ukitafuta kwa dhiki.
''
'' Sisi walipa ushuru, wajenga taifa, tena kwa bidii, twahangaishwa,
Tumenyimwa uhuru, tuna mbaya sifa, hatujivunii, tunapopotoshwa,
Kila tunapopazuru, damu na maafa, hatutulii, hali ya kutishwa
''
'' Vina Ubeti 1: ---ni, ---mi,
ubeti 2: ---ta, ---lo,
ubeti 3: ---po, ---wa,
''
'' vina Ubeti 1: ---shi, ---ma,
ubeti 2: ---shi, ---ko,
ubeti 3: ---shi, ---le,
ubeti 4: ---shi, ---pa
''
'' kwa mfano vina vikiwa ( ---ni, ---ka) kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.
''
'' Hakika tumeteleza, na njia tumepoteza,
Nani wa kutuongoza, aliyepewa uweza,
Filimbi akipuliza, tusiyeweza kupuuza,
Bali twaisikiliza, bila ya kuzungumza,
Bila ya kuzungumza, wala mwendo kulegeza,
Tumwandame ja mwangaza, kututoa palipo giza,
Penye dhiki ya kuliza, bila sauti kupaza
Pengo hili kulijaza, ni nani anayeweza, ''
'' Jiwe hili lala nini, ila moshi na majani,
Jiwe linalala lini, litokapo vileoni,
Jiwe hili halineni, lina macho halioni,
Jiwe na tulibebeni, tulitupe mitaroni
''
'' Nani binadamu yule, adumuye,
Anayeishi milele, maishaye
Jenezani asilale, aluliye,
Kaburi liko mbele, sikimbiye.
''
'' Hawajazawa warembo, usidhani umefika,
Ukisifiwa mapambo, jinsi ulivyoumbika,
Akipata jipya umbo, 'tabaki kihangaika,
Usidhani umefika. ''
Uchambuzi wa Mashairi
- Muundo/Umbo la shairi
- Uhuru wa Mshairi
- Maudhui
- Dhamira
- Mtindo wa / Mbinu za Lugha
Muundo/Umbo la Ushairi
Katika umbo wa shairi, tunaangazia jinsi shairi lilivyoundwa kwa kuangazia mizani, vina, mishororo n.k Aidha, ni muhimu kutaja aina na bahari za shairi zinazohusiana na kila sifa uliyoitaja.- Idadi ya mishororo katika kila ubeti - Tumia idadi ya mishororo kubainisha aina ya shairi hilo.
- Idadi ya mizani katika kila mshororo na katika kila kipande cha mshororo.
- Idadi ya vipande katika kila mshororo - Taja ikiwa shairi lina kipande kimoja, viwili, vitatu au vinne kisha utaje bahari yake.
- Kituo, kiishio au kibwagizo - Ikiwa mstari wa mwisho umerudiwa rudiwa, basi shairi lina kibwagizo au kiitikio, la sivyo lina kiishio.
- Vina - Zingatia vina vya kati na vya mwisho kutoka ubeti mmoja hadi mwingine. Kisha utaje ikiwa ni Mtiririko, Ukara au Ukaraguni
Uhuru wa Mshairi
Mshairi hafungwi na kanuni za kisarufi za lugha katika utunzi wa shairi. Anaweza kufanya makosa ya kisarufi kimakusudi ili shairi lizingatie umbo fulani. Zifuatazo ni njia mbalimbali ambazo mtunzi wa shairi anaweza kutumia kuonyesha uhuru wake.- Inkisari - kupunguza idadi ya silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.
- Mazda - kuongeza silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.
- Tabdila - kubadilisha silabi ya mwisho ili kustawazisha urari wa vina katika kipande bila kuathiri mizani.
- Kuboronga Sarufi -ni mbinu ya kupangua mpangilio wa maneno ili kuleta urari wa vina au mdundo wa ushairi.
- Utohozi - Kuswahilisha Maneno - Wakati mwingine mshairi anaweza kubadilisha neno la lugha nyingine litamkike kwa Kiswahili ili kudumisha mdundo wa kishairi na pia kupata neno mwafaka litakalotimiza arudhi za kiushairi.
Maudhui
Maudhui ni jumla ya ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika shairi fulani. Haya ni mambo yanayotajwa katika hadithi na yanaweza kujumuisha mawazo zaidi ya moja. Maudhui husaidia kujenga dhamira ya shairi.Dhamira
Dhamira ni lengo, dhumuni au nia ya mtunzi wa shairi. Mtunzi wa shairi anaweza kuwa na kusudi la kutuonya, kututahadharisha au kutunasihi kuhusiana na jambo fulani.Mtindo wa Lugha
Mtindo wa lugha hurejelea namna mbalimbali ambazo mshairi anatumia mbinu za lugha. Mshairi anaweza kutumia mbinu za lugha.Maghani Katika Fasihi Simulizi
Aina za Maghani
Zipo fani mbali mbali za maghani ambazo zimeainishwa katika tanzu mbili kuu:- Maghani ya Kawaida
- Maghani ya Masimulizi
Maghani ya Masimulizi
Lengo la maghani ya aina hii ni kusimulia kisa fulani, historia, n.k.Kuna fani mbili za Maghani ya Masimulizi:
a) Tendi
Tendi ni ushairi mrefu unaosimulia matukio ya kishujuaa. Tendi zinaposimuliwa huandamana na ala za muziki. Sifa za Tendi:- Ni ushairi mrefu
- Husimulia matendo ya kishujaa kwa njia kishairi
- Husimuliwa badala ya kuimbwa
- Huandamana na ala za muziki
- Husimulia visa vya kihistoria
- Hutungwa papo kwa hapo
b) Rara
Hizi ni hadithi fupi za kishairi zenye visa vya kusisimua, zinazosimuliwa zikiambatanishwa na ala za muziki. Aghalabu hughanwa na watoto; na hutumika kama michezo ya watoto. Sifa za Rara- Ni hadithi fupi za kishairi
- Husimulia visa vya kusisimua
- Zinaweza kuimbwa au kusimuliwa
- Huambatana na ala za muziki
- Aghalabu huwa ni visa vya kubuni
Maghani ya Kawaida (Sifo)
Maghani ya Kawaida ni maghani yanayosifia mtu, kitu au hali katika jamiia) Majigambo au Kivugo
Haya ni maghani ambayo mtunzi hujisifia (kujigamba) namna alivyo hodari katika nyanja fulani. Tungo hizi hutumia chuku na maneno ya kejeli kuwadunisha wapinzani wa mtunzi. Sifa za Majigambo- Hutumia nafsi ya kwanza
- Msimulizi hutumia maneno ya kujigamba
- Msimulizi hutumia chuku kwa wingi ili kujisifu
- Hutungwa kwa ubunifu mkubwa na hutumia mbinu kama sitiari, vidokezi, ishara n.k
- Majigambo mengi huwa mafupi, lakini baadhi yake huwa marefu.
- Huwa na matendo matukufu ya msimulizi
- Huwa na ahadi za matendo kutoka kwa msimulizi
b) Tondozi
Tondozi ni aina ya sifo ambayo husifia watu mashuhuri katika jamii kama vile viongozi Sifa za Tondozi- Huwa ni ushairi wa kusimuliwa
- Husifia mtu mwengine, mtu mashuhuri
- Hutumia chuku
- Hutumia mbinu kama sitiari, vidokezi, ishara n.k
- Hutaja matendo makubwa ya kiongozi anayesifiwa
Pembezi
Pembezi ni maghani ya kumsifu mpenzi. Sifa za Pembezi- Humsifu mpenzi wa mtu
- Aghalabu huwa ushairi mfupi
- Hutumia tamathali za lugha kwa wingi kama vile ishara kusimulia umbo la mpenzi
- Pembezi zinaweza kuandamana na ngoma
Comments
Post a Comment