Isimu Jamii
· Istilahi za Isimu Jamii
· Aina za Lugha
Istilahi za Isimu Jamii
· Isimu (linguistics) - ni mtalaa ambao huchunguza, huchanganua na pia kuchambua na kufafanua lugha kama mfumo wa mawasiliano baina ya wanadamu.
· Lugha - ni chombo cha mawasiliano baina ya watu. Lugha huzingatia mpangilio maalum wa sauti, maneno na sentensi.
· Sajili - ni mukhtadha/rejista mbalimbali au mitindo maalum ya lugha katika mazingira/hali mbalimbali. Mifano ya sajili ni kama vile lugha ya hospitalini, shuleni, sajili ya dini, biashara, kisiasa, michezo,
· Fonolojia - ni tawi la sayansi ya isimu linaloshughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti. Fonolojia hutumika kuunda alfabeti katika lugha fulani. Aghalabu kila lugha hutumia mfumo fulani wa sauti mahususi katika lugha hiyo pekee.
· Fonetiki - huchunguza sauti zinazotamkwa na binadamu bila kuzingatia lugha yoyote.
· Mofolojia - (au sarufi maumbo) ni tawi la isimu linalochunguza maneno ya lugha fulani, aina za maneno katika lugha, hasa upangaji wa mofimu mbalimbali zitumikazo kwa ajili ya kuunda maneno hayo. Kwa mfano, lugha ya Kiswahili hutumia mbinu kadhaa kuunda maneno kulingana na mpangilio wa mofimu. Kwa mfano, neno 'lima' linaweza kutumika kuunda maneno mengine katika Kiswahili k.m mkulima, kilimo, nimelima, limika n.k Katika kubadilisha mofimu hizi, tunaweza kubadilisha neno moja kutoka aina moja(kitenzi) hadi nyingine (nomino) n.k
· Sintaksi - (au sarufi miundo) ni tawi la isimu au taaluma ya sarufi inayoshughulikia jinsi vikundi vya maneno na sentensi mbalimbali zinajengwa katika lugha. Sintaksia huangazia kanuni au sheria za lugha. Kila lugha huwa na sheria zake za kuambatanisha maneno kama vile jinsi ya kufuatanisha vitenzi, nomino na vielezi. Kwa mfano: Mtoto yako shiba ni sentensi isiyokuwa na sintaksi. Sentensi sawa ingekuwa: Mtoto wako ameshiba.
· Semantiki - ni tawi la isimu linalochunguza maana halisia (mantiki) ya maneno, kifungu au sentensi katika lugha. Sentensi isiyokuwa na mantiki ni sentensi inayotoa maana ambayo haiwezekani katika uhalisia. Sentensi inaweza kuwa sawa kisintaksia lakini iwe na makosa ya kimantiki. Kwa mfano: Kiatu cha mbwa kimefutwa kazi kwa sababu kumi ni kubwa kama hewa.
Aina za Lugha Katika Isimu Jamii
1. Lafudhi - Ni upekee wa mtu katika matamshi (accent) unaoathiriwa na lugha ya mama, mazingira yake ya kijiografia au kiwango ujuzi wake wa lugha.
2. Lahaja - ni vijilugha vinavyoibuka kwa lugha moja kuu kutokana na tofauti za kijiografia baina ya wazungumzaji wa lugha hiyo. Kwa mfano lugha ya Kiswahili ina lahaja kadhaa kama vile Kimtang'ata, Kilamu, Kimvita, n.k. Tofauti baina ya lufudhi ni kama msamiati, muundo wa sentensi au matamshi.
3. Lugha rasmi - ni lugha inayotumika katika shughuli za kiofisi ama ya wakati wa mawasiliano rasmi katika taifa fulani. Kwa mfano, lugha rasmi nchini Kenya ni Kiingereza.
4. Lugha rasimi - ni mtindo wa lugha uliotumiwa na mtu/watu fulani mashuhuri (zamani) na ambao huonekana kuwa mtindo bora wa lugha unaofaa kuigwa na wengine. Kwa mfano lugha ya Shakespeare.
5. Lugha ya taifa - ni lugha inayoteuliwa na taifa fulani kama chombo cha mawasiliano baina ya wananchi, kwa maana inazungumzwa na wananchi wengi katika taifa hilo. Lugha ya taifa, nchini Kenya ni Kiswahili; Uganda ni Kiganda.
6. Lugha Sanifu - Ni lugha iliyokarabatiwa na sheria zake (k.v muundo wa sentensi, msamiati, sarufi, n.k) kubainishwa na kuandikwa, na kwa hivyo huzingatia sarufi maalum na upatanisho sahihi wa sentensi. Kwa mfano: Kiswahili sanifu - ni lugha isiyokuwa na makosa ya kisarufi.
7. Lingua Franka - Ni lugha inayoteuliwa miongoni watu wenye asili tofauti wasiozungumza lugha moja ili iwe lugha ya kuwaunganisha katika shughuli rasmi au za kibiashara.
8. Pijini - ni lugha inayozaliwa kutokana na mchanganyo wa lugha zaidi ya moja. Kwa mfano. Sheng' (lugha ya vijana mitaani nchini ni lugha iliyoibuka kutoka kwa Kiswahili na Kiingereza.
9. Krioli - Ni pijini iliyokomaa na kukubalika.
10. Lugha mame - hii ni lugha isiyokua na ambayo hubaki kati umbo lake la awali. Kwa mfano lugha ya Kilatini haibadiliki na hivyo hutumika katika kubuni majina ya kisayansi, n.k.
11. Lugha azali - ni lugha inayozaa lugha nyinginezo.
12. Misimu - ni lugha yenye maneno ya kisiri ambayo hutumiwa na kikundi fulani cha watu katika jamii, inayoeleweka tu baina yao. Misimu huibuka na kutoweka baada ya muda.
Sajili Katika Isimu Jamii
Kuna sajili anuwai za matumizi ya lugha katika jamii. Hapa tutazingatia mifano michache ya sajili mbali mbali.Kila sajili huwa na sifa mbalimbali zinazoitofautisha sajili hiyo na nyinginezo. Ili kubaini sifa za lugha katika sajili fulani, ni muhimu kuzingatia baadhi ya maswali yafuatayo:
· ni mazungumzo baina ya nani na nani?
· kuna uhusiano gani baina ya wanaozungumza?
· yanapatikana wapi?
· yanatumika katika hali gani?
· yana umuhimu ama lengo gani
· ni istilahi zipi istilahi (maneno maalum) zinazopatikana katika mazingira hayo?
· umaizi wa lugha baina ya wazungumzaji ni wa kiwango gani?
· ni mtindo gani wa lugha unaotumika?
MIFANO YA SAJILI
Sajili ya Ajali
Sifa za lugha inayopatikana katika sajili hii
1. Msamiati wa kipekee unaohusiana na ajali kama vile majeruhi, hudumanya kwanza, damu, mkasa.
2. Hutumia lugha ya kudadisi dadisi ili kubaini chanzo cha ajali.
3. Huwa na masimulizi – walio na habari kuhusu kisa hicho hueleza waliyoshuhudia
4. Kutokana na hali ya msukosuko, lugha hii haina utaratibu – watu huwa katika hali ya hofu, kwa juhudi za kuwaokoa majeruhi.
Mfano wa Sajili ya Ajali
Nimesikia twa! Kisha kishindo kikubwa sana (akihema hema) Nikaambia kuna mlipuko tukimbie. | |
Mwanakijiji 2: | Lilio la muhimu ni kuyaokoa maisha ya majeruhi kwa kuwapa huduma ya kwanza. |
Mwanakijiji 1: | Tuondoeni miili ya waliofariki kwanza. |
Mwanakijiji 2: | hatuwezi kuishika miili iliyobanwa katika gari hadi polisi wafike. Na ndio hao wanaokuja! |
Mwanakijiji 1: | (akikimbia) Ndio hao! Acheni kuiba mafuta! Polisi wanakuja! |
Polisi: | Wakitawanya wananchi walioliparamia gari kuiba bidhaa mbali mbali.Liinueni hili gari! Wapi dereva? |
Dereva: | (ambaye amelala akihema kwa maumivu, damu ikichuruzika miguuni na mikononi) Nilisitishwa na ng'ombe waliokuwa wakivuka barabara. Nilijsribu kukwepa lakini usukani ukanishinda gari likapoteza mwelekeo… |
Abiria: | Alikuwa akiendesha gari kwa kasi sana. Tukampigia kelele apunguze mwendo lakini hakutusikia. Matunda yake… |
Mwanakijiji 2: | Niliona gari likibingiria mara kadhaa mpaka likaingia humu mtaroni, ndiyo tukakimbia kuwaokoa. |
Polisi: | Nyamazeni! Achieni polisi kazi iliyobaki. Ikiwa kuna yeyote anayejuana na waathiriwa aandamane nasi. |
Sajili ya Biashara
Sifa za Lugha ya Biashara
1. Hutumia msamiati wa kibiashara kama vile:
o Fedha
o Faida
o Hasara
o Bei
o Bidhaa
2. Hutumia misimu ili kuwavutia wanunuzi
3. Ni lugha yenye malumbano hasa watu wanapojadiliana kuhusu bei
4. Ni lugha legevu - haizingatii kanuni za lugha.
5. Huchanganya ndimi kwa kuingiza maneno ya lugha za kigeni
6. Ni yenye heshima na unyenyekevu kwa wanunuaji
7. Msamiati katika lugha ya Kibiashara
Mfano wa Sajili ya Biashara
Tatu kwa mia! Tatu kwa mia! Leo ni bei ya hasara! | |
Mtu Y: | Unauza hii briefcase kwa pesa ngapi? |
Mtu X: | Hiyo ni seventy bob mtu wangu |
Mtu Y: | Huwezi kunipunguzia. Niuzie hamsini hivi. |
Mtu X: | Haiwezekani mtu wangu. NItapata hasara nikiuza hivyo. Ongeza mkwaja, mama. |
Mtu Y: | Basi hamsini na tano. |
Mtu X: | Tafadhali ongeza kitu kidogo. Unataka nikule hasara leo? Fikisha sitini na tano. |
Mtu Y: | Basi sitanunua hii. Sina pesa hizo zote. Unajua uchumi ni mbaya siku hizi. |
Mtu X: | Tafadhali mtu wangu. Huu mkoba ni mzuri sana. Umetoka Germany. Angalia. Unaweka pesa hapa, kitambulisho hapa halafu unafunga hivi. Hauwezi kupoteza chochote ukiwa na mkoba huu. Angalia wewe mwenyewe. Hakuna mahali pengine utaweza kununua mkoba huu kwa bei ghali kama hii. |
Mtu Y: | Nimekwambia sina hizo pesa. Nitanunua baadaye ukipunguza bei. |
Mtu X: | Lete sixty bob. Lakini utakuwa umeniumiza. Nakufanyia hivyo kwa kuwa wewe ni customer poa. |
Mtu Y: | Sawa basi nitanunua. Shika sixty bob. |
Mtu X: | Asante Customer. Mungu akubariki. (akimfungia) Hey! Tatu kwa mia. Bei ya hasara! Tatu kwa mia! |
Sajili ya Mtaani
Sifa za Lugha ya Mtaani
1. Ni lugha legevu isiyozingatia kanuni za kisarufi
2. Huchanganya ndimi
3. Hutumia misimu kwa wingi
4. Hukosa mada maalum
Mfano wa Sajili ya Mtaani
Hey, niaje msupaa? | |
Katosha: | Poa. So, mathee yako alikushow naweza kuja? |
Chali: | Ha! Masa hana noma. Si unajua nita... |
Katosha: | Chali! Unataka aniletee pr |
Sajili ya Bungeni
Sifa za Lugha ya Bungeni
1. Ni lugha yenye ushawishi – wabunge hutumia vishawishi ili kuwahimiza wenzao waunge ama kupinga msalaba
2. Ni lugha ya mjadala yenye waungao na wapingao.
3. Ni lugha yenye heshima na nidhamu. Maneno ya heshima kama mheshimiwa, tafadhali na samahani hutumika sana.
4. Hutumia maneno maalum yanayopatikana katika mazingira ya bunge kama vile kikao, mswaada, kuunga mkono, kujadili, kupitisha, n.k.
5. Lugha ya bungeni ni rasmi na sanifu.
6. Hulenga maswala mbalimbali ya kisiasa na maendeleo katika taifa.
7. Huwa na maelezo kamilifu
8. Ni lugha yenye maswali na majibu miongoni mwa wabunge.
Mfano wa sajili ya Bungeni
Waheshimiwa, muda unayoyoma. Nawaomba mfanye mazungumzo yenu sauti ya chini tumsikize huyu. Endelea mheshimiwa. | |
Mbunge 1: | Asante Bwana spika. Hii siyo mara ya kwanza ya kuuwasilisha mswaada huu hapa. Kila mbunge anayethamini raia wa taifa hili ni lazima auunge mkono mswada huu. Katika kikao kilichotangulia, mliupinga mkidai kwamba hauna heshima kwa rais. Leo tumefanya ukarabati wote mliotaka. Hamna budi kuuunga mkono. Bwana spika…. |
Spika: | Muda wako umekwisha tafadhali keti. Wabunge wataamua hatima ya mswada huu ikiwa utapitishwa kama sheria. Lakini kumbukeni uamuzi wa mwisho ni wa rais. |
Sajili ya Hospitalini
1. Hutumia msamiati wa hospitalini kama vile
o dawa
o magonjwa
o Daktari
o Wadi
o Mgonjwa
o Dawa
o Kipimo
2. Ni lugha yenye upole na heshima
3. Huwa na maswali mengi hasa daktari anapotaka kutambua kiini cha ugonjwa unaomhadhiri mgonjwa wake
4. Ni lugha yenye hofu na huzuni
Mfano wa Sajili ya Hospitalini
Ulianza kuumwa hivi lini? | |
Mgonjwa: | Kichwa kilianza kuniuma jana jioni baada ya chajio. Nilipoamka asubuhi nikatambua kwamba hata tumbo lilikuwa likiuma pia. |
Daktari: | Ulipoanza kuumwa na mwili mzima, ulichukua hatua gani? Hukunywa dawa yoyote? |
Mgonjwa: | Nilichukua tembe zilizokuwa zimepatiwa kakangu miaka mitano iliyopita alipokuwa akiumwa na malaria. |
Daktari: | Kila ugonjwa unahitaji matibabu mbalimbali. Tembe za malaria haziwezi kutumika kutibu maumivu ya kichwa na tumbo. Pia ni hatari kutumia dawa ambazo zimepitwa na wakati. Zinaweza kukuletea madhara zaidi. |
Mgonjwa: | (akikohoa) Sijui kama una tembe za kifua pia. Hii baridi inaniletea homa mbaya. |
Daktari: | Hatuwezi kukupatia dawa kabla ya kutambua ugonjwa ulio nao. Itabidi tupime joto lako, damu na pia mate yako ili kupata tatizo linalokusumbua. Kisha tutakupatia dawa. Je, una umri wa miaka mingapi? |
Mgonjwa: | Nikichukua hizo dawa nitapona? |
Daktari: | Matokeo hubadilika kutoka kwa mgonjwa mmoja hadi mwengine. Inaweza kuchukua muda. Huenda ukalazwa kwenye wadi kwa siku mbili tatu hivi. Umri wako, mama? |
Sajili ya Kidini
Sifa za Lugha ya Kidini
1. Hutumia msamiati wa kidini kama vile
o Bibilia
o maombi
o mbinguni
o jehanamu
o Madhabahu
o Paradiso
o Mbinguni
o Mwenyezi Mungu
o Mwokozi
2. Ni lugha inayonukuu sana hasa wazungumzaji wanaporejelea Kitabu kitakatifu
3. Lugha yenye heshima, upole na unyenyekevu
4. Lugha sanifu
5. Ni lugha iliyojaa ahadi nyingi kwa wanaoandamana na mafunzo ya kidini na vitisho kwa wanaoenda kinyume na mafundisho
6. Huwa imejaa matumaini
7. Ni lugha yenye kutoa maneno ya sifa, kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mfano wa Sajili ya Kidini
Bwana asifiwe Bi... | |
Bi Rangile: | Amina, mchungaji. Watoto wanaendeleaje? |
Boriti: | Karita hana neno. Mwenyezi Mungu ametunyeshea rehema na neema zake. Je, wajukuu wako wa hali gani? |
Bi Rangile: | Wanaendelea vizuri isipokuwa hawataendelea na masomo. Sijui nilimfanyia Mungu dhambi gani. |
Boriti: | Nasikitika sana kusikia hivyo. Mungu atawalinda mayatima hao. Yeye ndiye baba wa mayatima. Mungu ni mwenye huruma. |
Bi Rangile: | Sijui hayo, mchungaji. Hata sijui maana ya kuishi hapa duniani. Kila siku ni matatizo. |
Boriti: | Usife moyo. Mungu anasema katika kitabu cha Yohana 14:18, "Sitawaacha nyinyi kama mayatima..." Kwa hivyo, ukiwa na imani, Mungu atakuonekania. |
Bi Rangile: | Basi niombee mchungaji ili Saumu na Neema wapate karo ya kurudi shuleni. |
Boriti: | Funga macho tusali. Ewe Rabuka uliyejaa neema na baraka tele. Tunakushukuru na kulitukuza Jina lako takatifu kwa baraka zako za ajabu. Tunajua kwamba wewe ndiye Mungu uliyewatoa wana wa Israeli kutoka Misri. Sisi wenye dhambi tunakuja mbele yako tukiomba ukafanya miujiza katika nyumba hii ya Bi Rangile...... |
Wote: | Amina. |
Sajili ya Kisayansi
1. Hutumia msamiati wa kipekee unaoambatana na taaluma inayorejelewa.
2. Huwa na maelezo kwa ukamilifu.
3. Huwa na mpangilio maalum na maendelezo ya hoja na ujumbe.
4. Huchanganya ndimi na kutumia maneno ya kisayansi au lugha mbalimbali.
5. Hutumia lugha sanifu.
6. Ni lugha yenye udadisi mwingi (wakati wa kufanya utafiti)
Mfano wa Lugha ya Kisayansi
Kwa sababu zisizoweza kuepukika, kikundi chetu hakitamaliza utafiti ulioratibiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwezi ujao. Hii ni kwa sababu ya changamoto kadhaa ambazo tumekutana nazo. Kwanza, viluwiluwi, ambao ndio tunaotafiti wamekuwa haba sana wakati huu wa ukame. Pili, kutokana na kufungwa kwa maabara ya kisayansi katika taasisi hii, ni muhali kufanya majaribio yoyote ya kazi yetu. Tatu, kumekuwa na pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya wanakijiji kwamba kukusanya viluwiluwi kunawatia hofu. Aidha, tume yetu imepungukiwa na fedha baada ya serikali kusitisha kudhamini utafiti huu.
Baada ya kujadiliana kwa vikao tatu mfululizo, tume yetu inapendekeza haya: Muda wa kufanya utafiti uongezewe kwa kipindi cha miezi sita; serikali kupitia kwa taasisi hii ifadhili wachunguzi. Wananchi wahamasishwe kuhusu umuhimu wa kuwafanyia viwavi utafiti na maabara ya utafiti ikaraatiwe haraka iwezekanayo.
Baada ya kujadiliana kwa vikao tatu mfululizo, tume yetu inapendekeza haya: Muda wa kufanya utafiti uongezewe kwa kipindi cha miezi sita; serikali kupitia kwa taasisi hii ifadhili wachunguzi. Wananchi wahamasishwe kuhusu umuhimu wa kuwafanyia viwavi utafiti na maabara ya utafiti ikaraatiwe haraka iwezekanayo.
Sajili ya Mahakamani
Sifa za Lugha ya Mahakamani
1. Hutumia msamiati wa kipekee unaorejelea sheria kama vile
o katiba
o sheria
o mashtaka
o Hakimu
o Ushahidi
o Wakili
o Jela
o Mshitakiwa
o Kiongozi wa mashtakiwa
2. Huwa na maelezo marefu na ya kina ili kutafuta ushahidi wowote uliopo
3. Ni lugha yenye kunukuu sana hasa vipengele katika vitabu vya sheria kama vile katiba
4. Ni lugha rasmi na sanifu
5. Ni lugha iliyojaa maswali na majibizano
6. Ni lugha yenye heshima
Mfano wa Sajili ya Mahakamani
Musa Kasorogani, mwanaye Bi Safina na Mzee Mpotevu Kasorogani; umeshtakiwa kwa kosa la jaribio la mauaji mnamo tarehe 23/08 mwaka huu. Unaweza kukubali mashitaka, kukana au kunyamaza. Je, unakubali mashitaka. | |
Musa: | Naomba kukanusha mashtaka hayo, bwana mkubwa. |
Kiongozi: | Je, kuna shahidi yeyote katika kesi hii? |
Katili: | Hapa mkubwa. Siku hiyo ya tarehe 23/08, Musa alipatikana akiwa akijinyonga usiku wa maneno. Kijiji chote kilikusanyika hapo kwenye boma ya Kasorogani. Nilipoleta polisi, wakamkamata na kumpeleka hospitalini atibiwe kwanza. Ndiposa ameletwa hapa siku ya leo. |
Kiongozi: | Je, mshitakiwa una tetesi lolote. Ama pia unaweza kuleta wakili wako azungumze kwa niaba yako. |
Kisaka: | Bwana mkubwa, mimi ndiye wakili na shahidi wa Musa. Musa hakuua mtu. Alikuwa akijinyonga kutokana na mkasa uliomfika tarehe hiyo ya Agosti 23 baada ya bibi harusi wake kubadilika. Mimi na mamake, Bi Safina Kasorogani tulijaribu kumtuliza jioni hiyo. Asubuhi nilipoamka siku iliyofuatia, nikapata habari kwamba alikuwa amepelekwa hospitalini. Je, alipojaribu kujiua, alimwua mtu yeyote? |
Kiongozi: | Kulingana na katiba ya nchi hii, kifungu cha 12.ab, kuua ni kutoa uhai wa binadamu yeyote. Haijalishi ikiwa ni yeye mwenyewe au ikiwa ni rafiki yake. Hivyo basi jaribio la kujiua ni hatia kulingana na kanuni za nchi hii. Una jingine la kuulizia? |
Kisaka: | Je, sheria yetu inaruhusu mtu kuadhibiwa kwa kosa ambalo hakufanya? |
Kiongozi: | La hasha. |
Kisaka: | Basi tutakuwa tumekiuka kanuni za nchi yetu iwapo tutamhukumu Musa kwa kujiua ilhali hakujiua bado. Tunawezaje kutambua kama angekufa? |
Katili: | Inafaa ahukumiwe kinyonga au kifungo cha maisha gerezani. Hata alivunja simu yangu... |
Kiongozi: | Order! Lazima kutii mpangilio wa mahakama. Katili hauruhusiwi kuongea bila ruhusa ya hakimu au kiongozi wa mashitaka. Polisi, mpelekeni nje. |
Sajili ya Matanga
Sifa za Lugha ya Matanga/Mazishi
1. Hutumia msamiati wa maneno ya huzuni kama vile waombolezaji, makiwa, kifo, mauti, pole n.k.
2. Hutumia lugha ya kuliwaza/kufariji na kupa matumaini hasa kwa waombolezaji.
3. Ni lugha yenye unyenyekevu isiyotumia maneno yanayokera.
4. Hudhihirisha unyonge wa mwanadamu, kama asiye na mamlaka juu ya uhai wake.
5. Huwa na mbinu rejeshi kurejelea maisha ya marehemu alipokuwa hai.
6. Kwa mara nyingi hutumia maneno ya kusifu marehemu kutokana na aliyotenda.
7. Wakati mwingine huwa ni lugha inayodhihiri hali ya kukata tamaa.
Mfano wa Sajili ya Matangani
"Waombolezaji wenzangu, kama mnavyojua tumekusanyika hapa kwa ajili ya kumsindikiza rafiki yetu amabye amelala hapa. Ikiwa kuna mtu alifikwa zaidi na msiba huu ni mimi. Marehemu alikuwa rafiki wangu wa dhati tuliyeshirikiana naye sana. Nilimjua marehemu tukifanya kazi katika soko la Mauzoduni na tangu siku hiyo tumeishi kama ndugu; kuomba radhi ukikosewa; kusaidiana, na kadhalika. "
Habari za kifo chake zilinipiga kwa mughdha. Sikuamini kwamba amekufa; kwamba sitamwona tena aushini mwangu. Ninasikitika sana lakini kwa kuwa Mungu hakosi, ninaamini kwamba alimpenda zaidi ya tulivyompenda. Ombi langu kwa Mungu ni moja, kwamba amweke rafiki yangu mahali pema peponi; au popote alipojitafutia siku zake za uhai; nami nitakapokufa anipeleke papo hapo tuendelee kuwa marafiki. Mwenzangu lala. Lala salama tutaonana siku moja"
Habari za kifo chake zilinipiga kwa mughdha. Sikuamini kwamba amekufa; kwamba sitamwona tena aushini mwangu. Ninasikitika sana lakini kwa kuwa Mungu hakosi, ninaamini kwamba alimpenda zaidi ya tulivyompenda. Ombi langu kwa Mungu ni moja, kwamba amweke rafiki yangu mahali pema peponi; au popote alipojitafutia siku zake za uhai; nami nitakapokufa anipeleke papo hapo tuendelee kuwa marafiki. Mwenzangu lala. Lala salama tutaonana siku moja"
Sajili ya Michezoni
Sifa za Lugha ya Michezoni
1. Hutumia msamiati wa kipekee unaohusu michezo kama vile mpira, goli, mchezaji
2. Huchanganya ndimi na kuingiza maneno ya lugha nyingine kama vile Kiingereza. mfano 'goal!!!'
3. Ni lugha ambayo hutumia vihisishi na mshangao kwa wingi
4. Sentensi nyingi katika lugha hii huachwa bila kukamilika hasa hali inapobadilika uwanjani
5. Husimuliwa kwa haraka haraka ili kuambatana na kasi ya mchezo
6. Ni lugha yenye sifa na na chuku kwa mfano msimulizi anaposimulia sifa za mchezaji fulani
7. Hutumia misimu kama vile 'wametoka sare'
8. Hutumia kwa ya kulinganisha ili kuelezea matokeo ya mechi k.m 'walitoka mbili kwa nunge'
9. Ni lugha yenye kukariri (kurudia rudia) hasa mchezaji anapoumiliki mpira kwa muda mrefu au mwanariadha fulani anapoelekea kushinda katika mbio.
10. Huwa na sentensi fupi fupi
Mfano wa Sajili ya Michezoni
Nakwambia ndugu msikilizaji hapa mambo yamechacha kwelikweli. Hawa wachezaji wa Manyuu hawacheki na watu leo. Wameamua kuishambulia timu ya Cheusi bila huruma. Kumbuka kwamba hii ni mara yao ya... Lo! Anauchukua mpira pale, mchezaji nambari tisa... Matiksta. Matiksta, Matiksta na mpira. Anaucharazacharaza pale. Anamwangalia mwenzake. Anaupiga mpira kwa kichwa pale! Lo! Mwenzake anaukosa. Akiushika mpira pale ni mchezaji wa timu ya Cheusi, Romana. Romana, Romana anaelekeza mpira kwenye lango la Manyuu. Anaupiga mpira kwa nguvu! Lo! Hatari sana. Hatari sana katika lango la Manyuu. Hatari! hatari! Gooooaaaaaal! Noooo ooh! Wameukosa! Goal keeper ameudaka mpira huo. Pole sana wachezaji wa ... Mlinda lango anaupiga mpira huo kwa hasira. Juu kabisa. Anauchukua pale nambari saba, Saruta. Huyu ni mchezaji machahari sana. Mwaka uliopita, alipewa tuzo la mchezaji bora wa mwaka. Ananyang'anywa na mchezaji mwingine hapa. Wanakabiliana kidogo. Huyu mchezaji anaupiga mpira kwa mguu wa kushoto. Lo! Mpira umekuwa mwingi na ukatoka nje.
Mashabiki wa timu hizi mbili wanasubiri kwa hamu na ghamu kutambua ni nani atakayeibuka mshindi. Katika mechi zilizotangulia, timu hizi zimekuwa zikitoka sare. Lakini leo lazima mshindi atapatikana. Hawa ni fahali wawili. Kumbuka kwamba unapata matangazo haya moja kwa moja kupitia idhaa yako uipendayo, redio nambari moja kote nchini... Mpira unarudishwa uwanjani. Akienda kuurusha pale ni...
Mashabiki wa timu hizi mbili wanasubiri kwa hamu na ghamu kutambua ni nani atakayeibuka mshindi. Katika mechi zilizotangulia, timu hizi zimekuwa zikitoka sare. Lakini leo lazima mshindi atapatikana. Hawa ni fahali wawili. Kumbuka kwamba unapata matangazo haya moja kwa moja kupitia idhaa yako uipendayo, redio nambari moja kote nchini... Mpira unarudishwa uwanjani. Akienda kuurusha pale ni...
Comments
Post a Comment