Insha
- Insha za ubunifu
- Insha za kiuamilifu
Insha za kiuamilifu ni maandishi yenye mtindo maalum na hutumika katika mazingira halisi kwa kuzingatia mtindo huo rasmi. Kwa mfano kumbukumbu, resipe, barua, ratiba, n.k. Ubunifu wa mwanafunzi hauwezi ukaathiri mtindo wa insha hizi. Kwa hivyo anchohitajika zaidi kuzingatia ni mtindo wa utunzi mada na hoja muhimu.
Insha za Kubuni
Aina za Insha za Kubuni
- Insha za Mdokezo
- Insha za Methali
- Insha za Mada
- .
Insha za Mdokezo
Hizi ni Insha za ubunifu ambazo mwanafunzi hupewa kifungu cha maneno kinachopaswa kujitokeza katika insha yake.
Baadhi ya insha za aina hii huwa zimetangulizwa na mwanafunzi hutakiwa akamilishe na nyinginezo huwa na kimalizio. Japo mwanafunzi ana uhuru wa kuiendeleza insha yake atakavyo, ni sharti ajifunge katika maudhui yanayojitokeza katika mdokezo aliopewa. Kwa hivyo, kabla ya mwanafunzi kuiendeleza insha yake, ni sharti atambue maudhui yaliyokusudiwa na mtahini.
Kwa mfano:
Endeleza insha ifuatayo na uifanye iwe ya kuvutia:- Nikasikia sauti hiyo tena. Sikuamini masikio yangu. Moyo ukaanza kunienda mbio mbio. Mara upepo....
- Giza lilikuwa limechukua milki ya viumbe wote duniani. Nyota zilitoa mwanga hafifu na mwezi ulikuwa ushatua. Katika giza hilo la kaniki....
au
Andika insha inayoishia kwa dondoo hili...- ... na kuniacha machozi yakinienda mbilimbili.
- ... Hadi wa leo, juhudi zangu za kusahau matukio ya siku hiyo hazifui dafu.
Insha za Methali
Methali huwa na pande mbili na ni lazima insha ya methali izipe sehemu zote mbili uzito sawa. Upande mmoja hutoa wazo au pendekezo; na upande wa pili hutoa jibu, suluhisho au matokeo.
Chukua kwa mfano, "Mpanda ngazi hushuka". Katika insha yako ni lazima utoe hoja za kutosha kuonyesha kwamba mhusika fulani kweli alipanda ngazi (k.v alipata cheo kikubwa, alijisifu n.k). Mwandishi pia anapaswa kutoa hoja za kutosha kuonyesha namna mhusika huyo aliposhuka (k.v akafutwa kazi,n.k) . Kwa mara nyingi, wanafunzi huzingatia tu sehemu ya kwanza ya methali katika insha yote huku sehemu ya pili ikijitokeza katika aya ya mwisho pekee.
Kumbuka kwamba ni muhimu kuelewa maana ya methali vizuri kabla ya kuchagua insha ya methali.
Mifano ya Insha za Methali:Andika inayoonyesha ukweli wa methali ifuatayo. Ifanye insha yako iwe ya kupendeza.
- "Usiache mbachao kwa msala upitao"
- "Chururu si ndo ndo ndo"
- "Siku za Mwizi ni arobaini"
Insha za Mada
Hizi ni insha ambazo mwaandishi hutakiwa kuzungumzia mada fulani kwa kutoa hoja ama maelezo. Insha hizi hazimhitaji mtahiniwa kuanza kusimulia hadithi yake bali ni kurejelea mada aliyopewa. Mwandishi wa insha kama hii anapaswa kuwa na hoja za kutosha kuhusu mada aliyopewa kabla ya kuanza kuiandika. Hoja zote zinapaswa kujitokeza katika masimulizi yenye mtiririko wala si kuorodhesha hoja, moja baada ya jingine.
Kwa mfano:
Andika insha juu ya:- Umuhimu wa kupanda miti
- Athari za kuavya mimba
- Namna ya kuboresha kilimo katika sehemu zenye ukame
- Mbinu za kukabiliana na wezi wa mifugo.
Insha hizi huwa insha halisia na hivyo mwaandishi hawezi kupigia chuku au kutoa hoja zisizo kweli. Kwa mara nyingi insha hizi hurejelea maswala ibuka katika jamii k.v njaa, ukimwi, kilimo, ufisadi, ukabila, n.k
Hata hivyo mwanafunzi anaweza kupata insha za mada zinazohitaji ubunifu, mapambo ya lugha n.k. Angalia mifano ifuatayo.
Andika insha juu ya:- "Ndoto Niliyokuwa Nayo"
- "Siku Ambayo Sitaisahau Maishani"
- "Sherehe Niliyoihudhuria"
- "Ajali ya Barabarani Niliyoishuhudia"
Insha za Kiuamilifu
Hizi ni insha amabazo huchukua mtindo maalum wa kuandikwa. Japo mwanafunzi anaweza kubuni maudhui katika insha yake, hana uhuru wa kujichagulia muundo atakaotumia kuwasilisha utunzi wake bali anapaswa kuzingatia mtindo maalum wa kuandika insha hiyo.
Tumekuandalia Insha zifuatazo:INSHA MAELEZO KWA UFUPI Hotuba andika hotuba kwa hadhira kuhusu mada fulani Kumbukumbu rekodi za mkutano Resipe orodha ya viungo na maelekezo ya kuandaa chakula fulani. Ratiba mpangilio wa mambo katika shughuli fulani Mazungumzo majadiliano baina ya watu wawili au zaidi Mahojiano mazungumzo ambapo mtu mmoja anamhoji/kumwuliza maswali mwenzake Barua muundo wa barua rasmi, barua ya kirafiki na barua kwa mhariri Tahariri maoni ya mwandishi/mhariri Wasifu simulia maisha ya mtu mwengine Tawasifu simulia maisha yako mwenyewe Mjadala toa maoni yako kuhusu hoja fulani Insha za Barua
Kuna aina mbili za barua:
- Barua Rasmi
- Barua ya Kirafiki
Pia tutaangalia Barua Kwa Mhariri
Barua ya kirafiki
Barua ya kirafiki ni barua ambayo mtu huandika kwa mwenzake au mtu wa familia yake. Barua hii haichukui mtindo wowote maalum wa kuandikwa. Huwa na anuani moja tu: ya mpokeaji. Barua hii haitumii lugha rasmi na mwandishi anaweza kumrejelea mwandikiwa kwa kutumia jina lake la kwanza. Aidha barua za kirafiki haziitaji kutiwa saini.
Barua Rasmi
Barua rasmi au barua ya kiofisi/kibiashara huzingatia mtindo rasmi wa barua. Huwa na sehemu zifuatazo:
Muundo
- Anuwani ya mwaandishi huwekwa juu kabisa na huwa katika upande wa kulia wa kartasi.
- Tarehe ya barua hiyo - tarehe huandikwa chini ya anwani ya mwandishi
- Anuwani ya mpokeaji - Anwani ya anayeandikiwa huwa katika upande wa kushoto wa kartasi, na huwekwa msitari mmoja chini ya tarehe.
- Salamu-Chini ya anwani ya mpokeaji, barua huanza kwa kumrejelea mpokeaji kama bwana au bi. Ni makosa kumsalimia mpokeaji wa barua rasmi au kumwuliza hali yake.
Kwa Bwana Menomakubwa, => taja jina lake ikiwa mnajuana na unayemwandikia.
Kwa Bw/Bi, => Ikiwa humjui mpokeaji wa barua, tumia bw/bi - Mada -Kichwa cha barua rasmi huja pindi tu baada ya salamu. Hutangulizwa na maneno kama vile KUH:(kuhusu), MINT:(mintarafu). Ni sharti kiachwe kiandikwe kwa herufi kubwa na kipigiwe mstari. Kichwa kinapaswa kuwa kifupi na kinachoelezea mada ya barua kiukamilifu.
- Ujumbe - Ujumbe wa barua rasmi lazima uwe mfupi na unaotumia lugha rasmi.
- Tamati – mwandishi humalizia kwa maneno ya hitimisho kama vile:Wako mwaminifu,
[jina]
Sahihi
Barua kwa Mhariri
Hii ni barua ya msomaji wa jarida kwa mhariri mkuu wa jarida/gazeti fulani akitoa maoni yake kuhusu jambo fulani kama vile uchumi, kisa, sera za serikali au habari zozote zinazoendelea kwa wakati huo.
k.m:Kwa Mhariri Mkuu
Jarida la Mwenda Zake Leo
MINT : HATUA YA SERIKALI KUFADHILI SEKTA YA BODABODA
...ujumbe...Na [jina]
Hotuba
Insha ya hotuba ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/hatibu/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani. Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi halisi na mwandishi hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake.
Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika fulani, daktari, n.k. Hadhira katika hotuba husheheni wageni waalikwa, wanachama, wafuasi, wananchi, n.k ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa katika hotuba hiyo. Mengi ya maswala yanayojitokeza katika insha za hotuba ni maswala ibuka katika jamii k.v upangaji wa uzazi, usalama, n.k
Muundo wa Hotuba
Anwani
Anwani, mada au kichwa cha hotuba huchukua herejelea hatibu pamoja na mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja hadhira.
- Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa wananchi.
- Hotuba ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi
Utangulizi
- Anza hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano (hadhira).
- Wataje kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina pekee kunatosha.
- Jitambulishe kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia hadhira isiyokujua au wageni.
- Tanguliza mada yako. Kwa mfano:Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Chifu wa Kisioni, wanachama wa kikundi hiki cha Rotuba Bora, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi cha Mshipi wa Kijani Kibichi na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa ...
Mwili
- Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho
- Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.
Tamati
- Hakikisha kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
- Unaweza kumaliza kwa shukurani
Mfano ya Insha za Hotuba:
- Wewe ni chifu katika kijiji cha Kikanyageni. Andika hotuba utakayotoa kwa vijana kuhusu hatua za serikali kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya.
- Umealikwa kuwahutubia wanafunzi wa shule ya msingi uliyosomea kuhusu umuhimu wa elimu ya wasichana. Andika hotuba utakayotoa.
- Wewe ni daktari. Andika hotuba utakayotoa kuwahimiza wanawake wakubali kutumia mbinu za kupanga uzazi.
- Umeteuliwa na afisa katika idara ya utalii kuhutubia watalii kuhusu changamoto za kiusalama zinazolikabili bara hili na upendekeze mbinu za kuzitatua.
Insha za Kumbukumbu
Kumbukumbu za mikutano ni rekodi zinazowekwa na katibu wa mkutano mkutano unapoendelea ili kuhifadhi yanayojadiliwa na kukubalianwa katika mkutano huo. Katibu anapaswa kufuatilia mtindo maalum wa kuandika kumbukumbu hizo kulingana na mpangilio katika mkutano.
Muundo wa Kumbukumbu
1. Kichwa cha kumbukumbu
Kichwa cha kumbukumbu kinapaswa kutaja mambo yafuatayo:- Ni mkutano wa akina nani?
- Unaandaliwa wapi?
- Unaandaliwa lini?
- Unaanza saa ngapi?
2. Waliohudhuria
Andika orodha ya wote waliofika kwenye mkutano huku kuanzia na yule mwenye cheo cha juu zaidi hadi kwa wanachama. Pia onyesha vyeo vyao.3.Waliotoa Udhuru
Hawa ni wale walioomba ruhusa kutohudhuria mkutano ====
4.Waliokosa kuhudhuria
Hawa ni waliokosa kuhudhuria mkutano, bila kutoa udhuru)
5.Waalikwa
Hawa ni wageni walioalikwa katika mkutano, k.v mlezi wa chama, afisa wa kiutawala, n.k)
6. Ajenda
Orodhesha hoja zitakazorejelewa katika mkutano huoKUMB 1 | kumbukumbu ya kwanza huwa ni kufunguliwa kwa mkutano na ujumbe kutoka kwa mwenyekiti. |
KUMB 2 | Kusomwa kwa kumbukumbu za mkutano uliotangulia na kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo kwa kutiwa saini. |
KUMB 3 | Maswala yanayoibuka kutokana na kumbu kumbu zilizosomwa. (Kumbuka kutaja nambari ya kumbu kumbu hizo) |
KUMB 4 kuendelea | Maswala katika ajenda |
KUMB ya Mwisho | Maswala mengineyo yasiyokuwa kwenye orodha ya ajenda. |
Tamati | kufungwa kwa mkutano. Taja mkutano ulifungwa saa ngapi; mkutano ujao utakuwa tarehe ngapi; kisha acha nafasi ya kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo katika mkutano utakaofuatia. |
Mfano wa Insha ya Kumbukumbu
Waliohudhuria
- Thoma Mwororo - Mwenyekiti
- Vivian Mjaliwa - Mweka hazina
- Idi Baraka - Mkuu wa utafiti
- Fikra Mawimbi - mwanachama
- Mercy Rehema - katibu
Waliotuma Udhuru
- Bahati Sudi - Naibu Mwenyekiti
- Paul Kitanzi - Msimamizi wa Mijadala
Waliokosa Kuhudhuria
- Zakayo Chereko - Spika
- Juma Mtashi - mwanachama
Waalikwa
- Mdaku Mpelelezi - Mwanahabari
- Bw. Msawali - Mlezi wa Chama
- Uchapishaji wa jarida la Kiswahili
- Shindano la kuandika insha.
- Kusajili wanachama wapya
KUMBUKUMBU 1/04/10 - KUFUNGULIWA KWA MKUTANO
Mwenyekiti aliwakaribisha wanachama wote na baada ya kuwatambulisha wageni, akawaomba washiriki wawe huru kuchangia katika ajenda mkutano huu ili kuboresha chama.
KUMBUKUMBU 2/04/10 - KUREJELEA KUMBUKUMBU ZA MKUTANO ULIOPITA.
Katibu alisoma kumbukumbu za mkutano wa mwezi Machi. Kumbukumbu zilikubaliwa na wanachama wote na kuthibitishwa na mwewnyekiti pamoja na katibu kwa kutia saini.
KUMBUKUMBU 3/04/10 -MASWALA IBUKA KUTOKANA NA KUMBUKUMBU ZILIZOSOMWA
Mweka hazina alifahamisha mkutano kwamba aliongea na mkuu wa idara ya Kiswahili kuhusu ufadhili kama tulivyokuwa tumekubaliana katika KUMB 9/03/10 ya mkutano uliopita.
KUMBUKUMBU 5/04/10 - HAFLA YA KISWAHILI
Iliripotiwa kwamba hafla ya Kiswahili ambayo wanachama walikuwa wamealikwa kuhudhuria katika Shule ya Sakata Academy haingeweza kufanyika kutokana na tamasha za muziki zilizokuwa zinaendelea katika shule hiyo. Wanachama waliokuwa wamejitayarisha kwa mashairi waliombwa kuendelea kujifunza ili wayawasilishe muhula wa pili.
KUMBUKUMBU 4/04/10 - UCHAPISHAJI WA JARIDA LA KISWAHILI
Wanachama walikubaliana:-- Kwamba chama kitaanza kuchapisha jarida la Kiswahili
- Kwamba jarida litakuwa likichapishwa mara moja kila muhula na kuuzwa shuleni
- Kwamba kila mwanachama atachangia katika kuandika makala na kuuza nakala za jarida hilo.
- Kwamba paneli ya wahariri lingeundwa ili kuongoza idara ya uchapishaji
- Kwamba hazina ya chama ina fedha za kutosha kuzindua uchapishaji huo.
KUMBUKUMBU 5/04/10 - SHINDANO LA KUANDIKA INSHA
Kila muhula wa pili, chama huandaa shindano la kuandika insha ambalo wanafunzi wote hushiriki. Insha zilizopendekezwa mwaka huu ni:-- "Jadili chanzo cha migomo shuleni na namna ya kusuluhisha."
- ... ... ... ... ... ... ... ... ...
- ... ... ... ... ... ... ... ... ...
- ... ... ... ... ... ... ... ... ...
KUMBUKUMBU 6/04/10 KUSAJILI WANACHAMA WAPYA
... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ...
KUMBUKUMBU 7/04/10 MASWALA MENFINEYO
... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ... ...
KUFUNGWA KWA MKUTANO
Mkutano ulifungwa saa kumi na nusu, baada ya maswala yote kujadiliwa. Mkutano unaofuatia ulipoangwa kuwa tarehe ishirini mwezi Mei, katika Ukumbi wa Muziki.
KUTHIBITISHWA KWA KUMBU KUMBU
______________ | _____________ |
Mwenyekiti | Katibu |
Tarehe:________ | Tarehe:________ |
Insha za Mahojiano
Hizi ni insha ambazo mhusika mmoja huwa akimhoji au kumwuliza maswali mwenzake.
- Mahojiano ya mtu anayeomba kazi
- Mahojiano baina ya askari na shahidi kuhusu kisa cha mauaji
- Mahojiano baina ya mwaandishi wa habari na mwananchi kuhusu katiba mpya
- Mahojiano baina ya daktari na mgonjwa
Insha za Mazungumzo au Majadiliano
Hii ni insha ya mazungumzo baina ya watu wawili au zaidi. Ni lazima wahusika katika mazungumzo wajitokeze vizuri na sifa zao zitambulike. Hatutarajii watu katika mazungumzo wawe na fikira moja na usawa katika mapendekezo yao. Ukinzani au tofauti ya uteuzi wa maneno kati ya usemi wa mzungumzaji mmoja na mwengine ni lazima ijitokeze.
Mazungumzo yanaweza kuwa ya kutafuta suluhisho baina ya pande mbili zinazozozana kama vile mama na bintiye; kupanga jambo fulani, n.k
Insha ya Mazungumzo huandikwa katika usemi halisia, huku wasemaji wakionyeshwa kama vile mchezo wa kuigiza.
Vitendo vya wahusika huonyeshwa kwa mabano
Mfano wa Insha ya Mazungumzo
Mazungumzo baina ya Mwalimu Mkuu, Mwanafunzi na Babake kuhusu nidhamu ya mwanafunzi huyo.
Mwalimu: | Bwana Juma, nimekuita umchukue mtoto wako ukamsomeshe katika shule nyingine kwa maana amtushinda sisi. |
Mzazi: | Ikiwa amewashinda na ninyi ndio mlio na kiboko, si ataniua mimi! Hata mimi simtaki kwa maana simwezi. Hawezi kuja kwangu |
Juma: | Nimesema sitaki kusoma! Nimechosha na mtindo huu… |
Mzazi: | (akikunja shati)... ... |
Insha za Mjadala
Insha ya mjadala humhitaji mwanafunzi atoe maoni yake kuunga mada na pia kupinga kauli fulani. Katika insha za aina hii, mwanafunzi anaweza kuegemea upande mmoja tu ikiwa upande wa kupinga hauna hoja za kutosha.
Ratiba
Ratiba ni orodha ya mpangilio wa namna mambo yatakavyofuatana katika shughuli fulani. Lengo lake ni kuhakikisha wakati unatumiwa vizuri ili mambo fulani yasije yakakosa kutendwa kutokana na upungufu wa wakati.
Ratiba hutumika katika sherehe, mikutano, mazishi, hafla, tamasha, n.k
Sehemu za Ratiba
Kichwa
Kichwa cha ratiba hutaja mambo yafuatayo:- Shughuli yenyewe - Taja jina la tukio ambalo unaandalia ratiba. Kwa mfano Harusi ya Bwana na Bi Arusi, Siku ya Zawadi
- Tarehe ya shughuli - je shughuli hiyo itafanyika lini?
- Mahali- Taja mahali ambapo shughuli hiyo itafanyikia. kwa mfano katika uwanja wa michezo wa Kasarani, kanisa la St. Mtakatifu
- Ratiba ya Hafla ya Ukimwi katika Bustani la Uhuru tarehe tano Januari.
- Ratiba ya Mazishi ya Dkt. Marehemu tarehe 20/12/1923 Kijijini Vikwazoni
Mwili
Mwili wa ratiba hujumuisha mambo mbalimbali yatakayofanyika katika mpangilio maalum, saa mbalimbali. Ni vizuri kuzingatia vipengele vifuatavyo:- Saa - Onyesha saa ambazo tukio limepangiwa kuanza hadi linapotakiwa kumalizika
- Mahali - Ikiwa shughuli tofauti zinafanyika katika mahali mbalimbali kama vile vyumba tofauti, inapaswa hutaje mahali ambapo kila jambo litafanyikia.
- Wahusika - Taja mtu au watu waliopewa wajibu wa kutekeleza jambo fulani. Hii huwasaidia kujitayarisha ipasavyo.
Mfano wa Ratiba
RATIBA YA MAZISHI YA MZEE MAUTI TAREHE 20/12/1923 KIJIJINI MIZUKANI
SAA | SHUGHULI |
07: 00 | Marafiki wa Mauti watoa mwili kutoka SlowDeath Hospital |
10: 30 | Maombi katika kanisa la G.I.Z.A yakiongozwa na Pst. Muna Fiki |
11: 15 | Mwili kuwasilishwa nyumbani, familia ya Mauti |
12: 00 | Kupakuliwa kwa chakula na Bi Kamafisi, Bi Mwachafu na wapishi walioteuliwa |
1: 10 | Kukusanyika kwa umati |
2: 00 | Maombi ya kuanzisha shughuli za mazishi |
2: 30 | Shuhuda zikiongozwa na Mzee Siachwinyuma |
3: 00 | Ushuhuda wa serikali na Chifu Mtesi |
3: 40 | Kuteremshwa kwa mwili kaburini na vijana walioteuliwa |
4: 00 | Shukrani za Mwisho, na Mwenyekiti wa Chama cha Kufa Tukusaidie |
6: 00 | Kugawana mali ya marehemu, na wazee wa kijiji |
Resipe
Haya ni maandishi yanayotoa maagizo/maelekezo ya kuandaa chakula fulani.
Sehemu muhimu za resipe ni:
- Kichwa- Jina la mlo unaoandaa, Idadi ya watu wanaopikiwa
- Orodha ya viungo unavyohitaji- majina ya viungo, Idadi au kiasi kinachohitajika
- Maagizo/namna ya kupika
- Eleza kwa utaratibu kila hatua
- Taja wakati utakaotumika katika kila hatua.
- Hakikisha kila aina ya viungo ulivyotaja, inajitokeza katika maelezo ya kupika.
- Tamati
- Baada ya chakula kuiva, eleza kinaweza kupakuliwa na chakula kipi kinginecho k.v ugali na kitoweo cha kuku
Mfano
- Andika resipe ya kuandaa mchuzi wa kuku kwa watu watano.
- Andika resipe ya kuandaa chakula kwa mgonjwa wa moyo
Tahariri
Tahariri ni makala ya mhariri (mkuu) wa jarida/gazeti fulani. Mhariri mkuu hutoa maoni yake kuhusu mojawapo ya maswala ibuka. Sehemu kuu za tahariri ni:
- Jina la Gazeti/jarida
- Tarehe/nambari ya toleo hilo
- Mada ya Tahariri
- Ujumbe
- Jina la mwaandishi
Wasifu
Wasifu ni insha inayosimulia maisha ya mtu fulani tangu kuzaliwa kwake, elimu yake, kazi, ujuzi wake n.k. Anayeandika wasifu ni tofauti na anayezungumziwa katika wasifu huo.
Kuna aina tatu za wasifu:
- Wasifu wa Kawaida
- Tawasifu
- Wasifu-Kazi
Wasifu
Wasifu wa kawaida ni masimulizi ya maisha ya mtu fulani yanayosimuliwa na mtu mwengine. Kwa mfano, Wasifu Wa Siti Binti Saad ulioandikwa na Mwalimu Shaaban Robert.
Katika insha, mwanafunzi anawezaambiwa aandike wasifu wa:
- mtu mashuhuri- anayejulikana kama vile Nelson Mandela, Julius Nyerere au Mzee Jomo Kenyatta n.k
- mtu yeyote anayemjua - kama vile mzazi, rafiki, somo(kielelezo), mwalimu wake n.k
- mtu wa kubuni - mwanafunzi anaweza kubuni mtu na asimulie maisha yake
Tawasifu
Katika tawasifu, mwandishi huwa anasimulia maisha yake mwenyewe. Hivyo basi, tawasifu huandikwa na kusimuliwa katika nafsi ya kwanza.
Katika insha, mwanafunzi anaweza ulizwa asimulie:
- maisha yake binafsi
- maisha yake, miaka kadhaa ijayo
- maisha ya mtu fulani kama yake binafsi k.m ajifanye kuwa Rais wa Tanzania, halafu asimulie maisha yake tangu kuzaliwa hadi alipo. k.m 'Umekuwa Rais wa nchi yako kwa muda wa miaka mitano, andika tawasifu kuhusu maisha yako itakayowasaidia wananchi wako kukuelewa vyema zaidi
- maisha ya mhusika wa kubuni, kama yake binafsi
Wasifu-Kazi
Wasifu-kazi (Resume/Curriculum Vitae) ni stakabadhi inayotumiwa kuorodhesha mambo muhimu katika maisha ya mtu kama vile elimu, kazi, ujuzi n.k inayotumiwa sanasana katika kuomba kazi. Kinyume na wasifu na tawasifu ambazo hutumia lugha natharia (ya masimulizi), wasifu-kazi hutumia muundo fulani wa orodha na/au jedwali kuwasilisha mambo muhimu tu. Isitoshe, wasifu kazi huwa fupi - aghalabu ukrasa mmoja.
Tunapoorodhesha mambo fulani katika wasifu, tunaanza na yale ya hivi karibuni hadi yale ya kitambo. Kwa mfano, anza na shule uliyosomea mwisho, iliyokuwa imetangulia hiyo n.k hadi shule uliyoenda kwanza.
Muundo wa Wasifu-Kazi
Katika wasifu-kazi unahitajika kuonyesha:- Jina lako
- Namna ya mawasiliano (simu, anwani, barua pepe)
- Elimu
- orodhesha shule zote ulizozisomea kutoka shule uliyosomea mwisho hadi shule ile uliyoihudhuria kwanza.
- katika kila shule, onyesha miaka uliyohudhuria k.m 1996-2000
- onyesha shahada (degrees) na diploma ulizozipata
- Kazi
- orodhesha kazi zote ulizozifanya kutoka kazi ya hivi karibuni hadi kazi ulizozifanya mwanzoni
- onyesha cheo ulichokuwa nacho katika kazi hiyo na majukumu yake
- onyesha kampuni au mahali ulipofanya kazi hiyo
- onyesha miaka ambayo ulikuwa katika kazi hiyo
- taja ujuzi au taaluma uliyoipata katika kazi hiyo
- Ujuzi / Taaluma - taja ujuzi maalumu ulionao, taaluma au talanta zozote zinazokufanya
- Mapato/Mafanikio/Tuzo - taja mafanikio yoyote au tuzo zozote ulizozipata katika maisha
- Mapendeleo - Nini kinakupendeza katika maisha? unapenda kutumiaje muda wako wa likizo usiokuwa wa kazi
- Maono ya Kazi - una maono gani katika kufanya kazi? ungependa kufanya nini?
Angalia hapa baadaye kwa mfano wa wasifu-kazi.
Comments
Post a Comment