Fasihi
Tanzu za Fasihi
Kuna tanzu mbili kuu za fasihi, na kila utanzu una vipera vyake: Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi:Fasihi Simulizi
- Hadithi (Ngano) - hekaya, mighani, visasili n.k
- Nyimbo - za jandoni, za ndoa, za kazi n.k
- Maigizo - michezo ya kuigiza, ngomezi n.k
- Tungo Fupi - methali, vitendawili n.k
Fasihi Andishi
- Hadithi Fupi - hadithi isiyokuwa ndefu iliyochapishwa katika mkusanyiko wa hadithi nyingine
- Riwaya - hadithi ndefu iliyochapishwa katika kitabu chake pekee
- Tamthilia - mchezo wa kuigiza uliowekwa kwa maandishi
- Ushairi* - mashairi yaliyoandikwa
Tanbihi:Ushairi ni kipera cha nyimbo lakini pia mashairi yanaweza kuwa chini ya Fasihi Andishi, ikiwa yamechapishwa.
Tofauti kati ya Fasihi Andishi na Fasihi Simulizi
FASIHI SIMULIZI | FASIHI ANDISHI | |
1. | Huwasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo. | Huwasilishwa kwa njia ya maandishi |
2. | Ni mali ya jamii. | Kazi andishi ni mali ya mwandishi (na mchapishaji) |
3. | Msimulizi anaweza kubadilisha sehemu fulani | Kitabu kilichoandikwa hakiwezi kubadilishwa |
4. | Huhifadhiwa akilini | Huhifadhiwa vitabuni |
5. | Kazi simulizi hubadilika na wakati | Kazi andishi haibadiliki na wakati |
6. | Huhitaji msimulizi na hadhira yake wawe mahali pamoja wakati wa masimulizi | Msomaji anaweza kusoma kitabu cha hadithi peke yake, mahali popote, wakati wowote |
7. | Mtu yeyote anaweza kutunga na kusimulia | Ni lazima mwandishi na msomaji wawe na uwezo wa kusoma |
8. | Hutumia wahusika changamano (wanyama, watu, mazimwi n.k) | Hutumia wahusika wanadamu. |
Umuhimu wa Fasihi Katika Jamii
- Kuburudisha jamii. Takribani vipera vyote vya fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira.
- Kuelimisha. Fasihi hukusudia kuelimisha hadhira kuhusu jamii, mazingira n.k
- Kudumisha maadili katika jamii kwa kuelekeza, kuonya na kunasihi hadhira jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
- Kuunganisha jamii. Fasihi huleta pamoja watu katika jamii. Kwa mfano, katika nyimbo, miviga, vichekesho.
- Kukuza lugha. Aghalabu tungo zote za fasihi hutumia lugha. Isitoshe, fasihi hutumia mbinu nyingi za lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na ukwasi wa lugha.
- Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Aghalabu kazi za fasihi (hasahasa Fasihi Simulizi) huambatanishwa na desturi mbalimbali za jamii husika.
- Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. k.m vitendawili, ngano za mtanziko n.k
Ngano Katika Fasihi Simulizi
Vipera vya Ngano
Tunaweza kuainisha ngano kulingana na vipengele vifuatavyo:- Wahusika => k.v khurafa, hekaya, mighani, mazimwi,
- Maudhui => k.v usuli, visasili, mtanziko
AINA | MAELEZO KWA UFUPI |
Khurafa | hadithi ambazo wahusika ni wanyama. |
Hekaya | mhusika mmoja (k.v sungura) huwa mjanja kuliko wenzake |
Usuli (Visaviini) | huelezea chanzo cha jambo au hali fulani |
Visasili | huelezea asili au chimbuko la jamii au mambo ya kiada k.v mauti, ndoa, tohara n.k. |
Mighani (Visakale) | hadithi za mashujaa |
Mazimwi | huwa na wahusika majitu au mazimwi |
Mtanziko | humwacha mhusika katika hali ya kutojua chaguo linalofaa. Kila achagualo lina matukio mabaya. |
Sifa za Ngano
- Huwa na mianzo maalumu
- Paukwa! Pakawa!
- "Hadithi! Hadithi!" - "Hadithi Njoo!"
- Hapo zamani za kale...
- Huwa na miishio maalum
- Hadithi yangu yaishia papo!
- ...wakaishi kwa raha mustarehe.
- Huwa na funzo fulani ambalo aghalabu hutajwa mwishoni mwa hadithi.
- Masimulizi yake huwa kwa wakati uliopita
- Husimuliwa kwa lugha ya natharia
- Huwa na wahusika ambao wanaweza kuwa binadamu, wanyama, miungu, mashetani au vitu visivyo hai
- Huhusisha mbinu nyingine za fasihi simulizi kama vile
- Nyimbo - kuburudisha, kuamsha hadhira, kupitisha ujumbe
- Methali - kutoa funzo
- Misemo - kupamba lugha
- Vitendawili na mafumbo - kushirikisha hadhira katika masimulizi
- Hutumia mbinu ya takriri ili kusisitiza ujumbe kwa kurudiarudia maneno, matukio au nyimbo
- Hutumia tamathali za lugha kama vile tashbihi, tashihisi, chuku, tanakali za sauti ili kupamba masimulizi n.k
- Huwa na muundo rahisi wenye mwanzo, kati na mwisho.
- Ufanisi wake hutegemea mbinu za mtambaji k.v ishara-uso na ubunifu wake jukwaani.
- Sehemu fulani zinaweza kubadilishwa kulingana na hadhira
Umuhimu wa Ngano
- Kuhifadhi au kurithisha mali ya jamii
- Kuunganisha na kukuza ushirikiano miongoni mwa jamii
- Kuelemisha au kutoa mafunzo kuhusu mambo fulani
- Kukuza maadili mema
- Kuonya, kuelekeza, kuhimiza na kunasihi
- Kuburudisha hadhira. Hadithi nyingi huwa na visa vya kusisimua na kuburudisha.
- Kupitisha muda haswa watoto wanaposubiri chakula kiive
Sifa za Mtambaji wa Hadithi
Msimulizi wa hadithi pia huitwa mtambaji, fanani au mganaji.- Huwa mchangamfu na mcheshi kwa hadhira yake ili kuwafanya wapendezwe na hadithi
- Anafahamu utamaduni wa jamii yake.
- Anaifahamu hadhira yake vizuri na kusimulia kulingana na mapendeleo yao. wasichana au wavulana? vijana au wazee?
- Huwa na uwezo wa ufaraguni - uwezo wa kubadilisha sehemu fulani za sanaa bila kujifunga na muundo asilia.
- Mwenye kumbukumbu nzuri - uwezo wa kukumbuka
- Mwenye uwezo wa kuigiza kwa kutumia viungo vyake, uso (ishara-uso) na sauti(kiimbo)
- Mwenye uwezo wa kujenga taharuki kwa kusita kidogo ili kuvuta nadhari ya hadhira yake.
- Hushirikisha hadhira yake katika nyimbo n.k
- Mlumbi hodari na mkwasi wa lugha.
Nyimbo Katika Fasihi Simulizi
Aghalabu nyimbo hutumia ala za mziki kama vile ngoma. Nyimbo zinaweza kuimbwa na mtu mmoja au zaidi.
Wimbo hugawanywa katika beti na mishororo. Nyimbo nyingi huwa na kiitikio au mstari ambao hurudiwa rudiwa.
Sifa za Nyimbo
- Hutumia kiimbo au sauti maalum
- Huweza kuendamana na ala za muziki
- Huimbwa na mtu mmoja au watu wengi; wakati mwingine nyimbo huimbwa kwa kupokezanwa.
- Hutumia lugha ya mkato
- Hurudiarudia (kukariri) maneno ili kusisitiza ujumbe katika wimbo
Umuhimu wa Nyimbo katika Fasihi Simulizi
- Kuburudisha
- Kuelimisha, kufunza, kuonya, kuelekeza
- Kuliwaza
- Kusifia kitu au mtu katika jamii
- Kuunganisha jamii
- Kudumisha/kuhifadhi tamaduni za jamii
- Kukuza talanta na sanaa katika jamii
- Hutumika katika mbinu nyingine za fasihi kama vile hadithi
Vipera/Aina za Nyimbo
Kulingana na Muundo:
- Mashairi
- Maghani
Kulingana na Ujumbe/Maudhui:
Nyimbo za Ndoa
Nyimbo za harusi huimbiwa bwana na bibi harusi kuwapongeza na kuwapa heko kwa kufunga ndoa yao. Aidha nyimbo hizi huwapa wawili hao mawaidha ya kutunza familia na watoto wao ili waishi pamoja.Nyimbo za Jandoni/Tohara
huimbwa na vijana wanapopashwa tohara. Nyimbo hizi huonyesha ushujaa, na kuashiria kutoka kwamba anayetahiriwa amekuwa mtu mzima sasa.Hodiya/Wawe
Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na watu wanapofanya kazi ili kuwatia bidii wafanye kazi bila kuhisi machofu.Kimai
Nyimbo za Mabaharia - Hizi ni nyimbo za wanabahari wanaposafiri baharini.Nyimbo za Mazishi/Huzuni/Simanzi
Hizi ni nyimbo za kuliwaza na kuwapa pole walioachwa na marehemu. Nyimbo hizi huwapa matumaini waombolezaji.Nyimbo za Kidini
Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa kumsifia Mungu, kuomba au kutoa mafunzo ya kidini.Nyimbo za Kisiasa
Hizi ni nyimbo za kuwasifia viongozi wa kisiasaNyimbo za Kizalendo
Nyimbo za huonyesha uzalendo kwa kusifia taifa/nchiNyimbo za Mapenzi
Katika nyimbo za mapenzi, mwimbaji huimba kwa kumsifia mpenzi wake hasa kwa urembo na tabia zake.Maigizo
Mifano:Tungo Fupi ni kipera cha Fasihi Simulizi kinachojumulisha sanaa simulizi zinazoundwa kwa maneno machache; sentensi moja au mbili hivi. Tungo Fupi nyingi huwa na sehemu mbili na aghalabu huhitaji kujibizana ambapo mtu mmoja hutoa pendekezo au swali; halafu mtu mwengine hutoa jawabu - k.m vitendawili na mafumbo. Baadhi ya tungo fupi husemwa na mtu mmoja tu kama vile methali.
Aghalabu vipera vyote vya tungo fupi hutumiwa katika kazi nyingine za fasihi ( na lugha kwa ujumla ) kama mapambo ya lugha.
Hadithi Fupi ni aina ya kazi andishi ambayo huwa fupi; na huangazia wazo moja kwa kurejelea kisa kimoja. Hadithi huwa na wahusika wachache na huchukua muda mfupi. Aghalabu hadithi fupi huchapishwa katika mkusanyiko wa hadithi nyingine fupi.
- Michezo ya Kuigiza (Jukwaani) - Haya ni maigizo ya jukwaani ambapo watendaji huiga maneno na matendo ya wahusika mbele ya hadhira.
- Miviga - Miviga ni sherehe mbalimbali katika jamii fulani. Watu hujumukika na sherehe hizi kulingana na tamaduni zao
- Ngomezi - ni sanaa ya ngoma. Midundo mbalimbali ya ngoma hutumika kuwasilisha ujumbe mbalimbali.
- Malumbano ya Utani - Malumbano ya utani ni mashindano ya kuongea jukwaani baina ya watu wa makundi au jamii mbili ambayo hutumia kejeli na chuku kukejeli tabia mbaya katika jamii au kundi fulani
- Ulumbi - Ulumbi ni uwezo wa kipekee wa kuzungumza mbele ya hadhira. Mtu mwenye uwezo huo wa kipekee wa kuzungumza jukwaani huitwa mlumbi.
- Soga - Soga ni mazungumzo baina ya watu wawili au zaidi ambayo aghalabu huwa hayana mada maalum.
- Vichekesho - Vichekesho ni aina ya sanaa ya fasihi simulizi ambayo watu hutoa vihadithi vifupi au sentensi zenye uwezo wa kuwafanya wasikilizaji wacheke.
- Maonyesho ya Sanaa - Maonyesho huhusisha watu wa jamii au kundi fulani wanaoonyesha taaluma, ujuzi au sanaa yao kwa watazamaji.
Tungo Fupi
Aghalabu vipera vyote vya tungo fupi hutumiwa katika kazi nyingine za fasihi ( na lugha kwa ujumla ) kama mapambo ya lugha.
Vipera vya Tungo Fupi
- Methali
Methali ni tungo fupi za sentensi moja ambazo hutoa funzo fulani kwa njia ya mafumbo. Methali huwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza hutoa hoja nayo sehemu ya pili hutoa suluhisho. Methali hutumika kwa minajili ya kutoa funzo kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Methali nyingine huhitaji hekima ili kujua maana yake. - Vitendawili
Vitendawili ni tungo fupi ambazo huwa na swali fupi na jibu kwa makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa kitendawili huulizia swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea umbo la kitu hicho, sauti, harufu au kukifananisha na kitu kingine. Anayejibu huhitajika kufikiria haraka na kutoa jawabu ambalo huwa la neno moja au maneno mawili hivi. Vitendawili huwa na mianzo maalum kulingana na jamii yake. - Mafumbo
Mafumbo hutumika kuupima uwezo wa mtu kufikira na kufumbua swali ambalo huwa na maelezo marefu. Majibu ya mafumbo huhitaji maelezo na aghalabu hukusudia kujua jinsi mtu anavyoweza kutatua tatizo fulani ambalo linahitaji kufikiria sana. - Vitanza Ndimi
Vitanza ndimi huwa ni sentensi zinazotumia maneno yanayomkanganya msomaji katika matamshi. Vitanza ndimi huhitaji kutamkwa haraka haraka na kurudiwa rudiwa mara kadhaa kwa kusudi la kukuza uwezo wa kutamka. - Vichezea Maneno
Ni maneno yanayokaribiana kimatamshi au kimaana hutumika katika sentensi moja kama njia ya kuonyesha ukwasi wa lugha au kuburudisha. Pia hutumika kama vitanza ndimi. - Misimu
Misimu ni maneno ambayo huzuka miongoni mwa kundi fulani katika jamii na hueleweka tu miongoni mwa watu katika kundi hilo. Misimu hukua na kutoweka baada ya muda. - Lakabu
Lakabu ni majina yanayobandikwa watu kutokana na sifa zao, maumbile, hulka au mambo yanayowahusu. Lakabu pia ni mbinu ya sanaa. - Semi (Nahau na Misemo)
Semi ni mafungu ya maneno ambayo hutumika kuleta maana tofauti na maana halisi ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha maneno makali kwa kutumia maneno mengine. Aidha semi zinaweza kutumika tu kwa minajili ya kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi: Nahau na misemo
Fasihi Andishi
Fasihi Andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno yaliyoandikwa kupitisha ujumbe. Ni sanaa inayopitishwa kwa njia ya maandishi
Tanzu za Fasihi Andishi
Kuna tanzu nne kuu za Fasihi Simulizi:- Hadithi Fupi - kazi andishi ya fasihi isiyokuwa ndefu sana
- Riwaya - kazi andishi ya fasihi ambayo huwa ndefu kuliko hadithi fupi
- Tamthilia- kazi andishi ya fasihi inayowasilisha mchezo wa kuigiza
- Mashairi - mashairi yaliyochapishwa huwa chini ya fasihi andishi.
Sifa za Fasihi Andishi
- Hupitishwa kwa njia ya maandishi
- Ni mali ya mtu binafsi
- Haiwezi kubadilishwa
- Hutumia mbinu za lugha na mbinu za sanaa
Umuhimu wa Fasihi Andishi
- Kuhifadhi kazi ya sanaa katika maandishi
- Kukuza lugha
- Kuburudisha
- Kuelimisha
- Kukashifu tabia zisizoandamana na maadili ya jamii
- Kuonya, kuelekeza, kunasihi
Uchambuzi wa Fasihi Andishi
Unapochambua kazi ya fasihi andishi zingatia:Aina ya Kazi Andishi
- Tambua aina au kipera cha kazi andishi ikiwa ni riwaya, hadithi fupi au tamthilia
Wahusika
- Tambua wahusika katika kazi hiyo ya fasihi
- Fafanua sifa za kila mhusika kwa kutumia vivumishi au virai vivumishi vinavyolingana na hulka za mhusika huyo.
- Aidha, unapaswa kuyakinisha sifa hizo kwa kutolea mifano kutoka kwenye hadithi
- Taja aina ya wahusika
Maudhui na Dhamira
- Maudhui - ni nini kinachofanyika?
- Dhamira - lengo/kusudi la kazi hiyo ni nini?
Mandhari
- Hadithi inafanyika katika mazingira gani?
- Mazingira hayo yanachangia vipi katika kisa hicho au sifa za wahusika?
- Msanii ameunda hali gani? (hisia, n.k)
Mbinu za Lugha
- Taja kwa kutolea mifano, fani za lugha zilizotumika ili kuifanya lugha iwe ya kuvutia zaidi
- Fafanua mbinu za sanaa zilizotumika na utaje mifano mwafaka
Hadithi Fupi
Mifano ya Hadithi Fupi
Hadithi Fupi kutoka kwenye mkusanyiko wa hadithi katika Mayai Waziri Wa Maradhi na Hadithi Nyinginezo- "Kachukua Hatua Nyingine"
- "Mayai Waziri wa Maradhi"
- "Siku ya Mganga"
- "Ngome ya Nafsi"
Tofauti kati ya Hadithi Fupi na Riwaya
HADITHI FUPI | RIWAYA | |
1. | Huwa fupi - hadithi fupi nyingi huhitaji kuunganishwa pamoja kuunda kitabu kimoja. | Huwa ndefu - huunda kitabu kizima |
2. | Huwa na wahusika wachache. | Huwa na wahusika wengi |
3. | Hurejelea wazo au kisa kimoja tu | Huwa na visa vingi na mawazo mengi yanayojenga wazo kuu |
4. | Husimuliwa kwa lugha ya moja kwa moja | Masimulizi yake yanaweza kuchanganya visengere nyuma na visengere mbele. |
5. | Huwa na muundo rahisi kueleweka | Aghalabu huwa vigumu kueleweka |
6. | Hufanyika katika mandhari/mazingira moja tu au chache. | Visa mbalimbali hufanyika katika mandhari mbalimbali |
Riwaya
Aina za Riwaya
Kunazo aina kadhaa za Riwaya katika Fasihi Andishi:- Riwaya sahili - visa vyake husimuliwa moja kwa moja na huwa rahisi kueleweka
- Riwaya changamano - hii ni riwaya ambayo huhitaji kusomwa kwa makini ili kueleweka. Aghalabu huwa na maudhui mengi na wahusika wengi ambao wanachangia katika tatizo kuu katika riwaya hiyo. Hujengwa kwa taharuki ili kuwavutia hadhira kutazamia jinsi tatizo kuu litakavyotatuliwa. Hutumia mbinu za taharuki na visengere nyuma/mbele.
- Riwaya ya kibarua - hutumia muundo wa barua kuwasilisha ujumbe wake.
- Riwaya kiambo - huhusisha maswala ya kawaida katika jamii
Mifano ya Riwaya
- Utengano
- Siku Njema
- Mwisho wa Kosa
- Kiu
Tamthilia
Aina za Tamthilia
Kunazo aina kadhaa za tamthilia katika fasihi andishi:- Tamthilia Cheshi/Komedia - ni mchezo wa kuchekesha. Maudhui yake huundwa kwa lengo la kutumbuiza hadhira.
- Tamthilia Simanzi/Trejedia - ni mchezo uliojaa huzuni, mikasa, mikosi, visa vya kutisha na aghalabu baadhi ya wahusika wakuu hufa.
- Tamthilia Simanzi-Cheshi/Trejikomedia - ni mchezo wenye visa vya kuhuzunisha lakini pia unawasilisha kwa njia ya kuchekesha. Aghalabu wahusika hutumia kejeli kuchekesha hadhira ijapokuwa kuna shida fulani inayowakabili. Baadhi ya wahusika wakuu hukumbwa na mikasa.
Mfano: Kifo Kisimani (na Kithaka Wa Mberia) - Tamthilia Tatizo - ni mchezo wa kuigiza ambapo wahusika huwa na tatizo/shida kuu wanalotaka kulitatua. Tamthilia hii aghalabu hutumia mbinu ya taharuki ili kuwafanya hadhira wawe makini ili kuona jinsi tatizo hilo litakavyoishia.
- Tamthilia ya Domestiki Drama - ni mchezo unaoangazia maisha ya kawaida ya watu kama vile familia, urafiki, ndoa n.k
- Tamthilia ya Melodrama - ni mchezo ambao husisitiza sifa za wahusika kwa kuunda wahusika kuunda wahusika wenye sifa zilizopigiwa chuku na zisizobadilika. Tamthilia hizi huundwa kwa namna inayowafanya hadhira wawapende wahusika fulani na wawachukie wahusika wengine. Kwa mfano:
- Shujaa ambaye hushinda kila mara
- Wahusika wabaya ambao hubakia wabaya kutoka mwanzo hadi mwishi
- Wahusika wazuri ambao hufanya vitendo vizuri kutoka mwanzo hadi mwisho
- Wapenzi ambao hata wakitenganishwa bado watapendana
- Aghalabu huishia kwa raha mustarehe
Mifano ya Tamthilia
- Kifo Kisimani
- Shamba la Wanyama
- Mstahiki Meya
Wahusika Katika Fasihi Andishi
Aina za Wahusika
- Wahusika Wakuu ⇒ hawa ni wahusika ambao wanahusishwa na takribani visa vyote katika riwaya/tamthilia. Wahusika huhusishwa kutoka mwanzo hadi mwisho. Aghalabu mhusika mkuu hafi isipokuwa katika trejedia/simanzi au hufa kifo cha ushujaa.
- Wahusika Wasaidizi ⇒ hawa ni wahusika wanaosaidia kujenga mhusika mkuu. Hutokeza mara nyingi katika hadithi. Wahusika wasaidizi wanaweza kuwa na visa vyao. Kwa mfano marafiki na aila za wahusika wakuu.
- Wahusika Wadogo ⇒ ni wahusika ambao wanafanya kazi ndogo sana katika fasihi kama vile kujenga maudhui au mandhari. Wahusika hawa wakitolewa, riwaya/tamthilia inaweza kuendela bila kubadilika sana. Kwa mfano mwenye duka ambalo mhusika alinunua kitu fulani.
- Wahusika Bapa ⇒ hawa ni wahusika wasiobadilika kutoka mwanzo hadi mwisho. Kwa mfano, mhusika mbaya anabakia kuwa mbaya kutoka mwanzo hadi mwisho. Sifa za wahusika bapa huweza kutambulika mwanzoni mwa hadithi/riwaya. Wahusika bapa hawawakilishi sifa halisia za binadamu. Nia yao ni kujenga tabia moja tu.
- Wahusika bapa-sugu - huoenyesha msimamo wao kulingana na masimulizi ya msanii.
- Wahusika bapa-vielelezo - msimamo wao hutambulika kulingana na majina yao. Msanii hutumia mbinu ya majazi au lakabu kuwapatia wahusika majina yanayolingana na sifa zao. Kwa mfano: Mhusika Rehema ni mwenye huruma na neema kutoka mwanzo hadi mwisho.
- Wahusika Duara ⇒ mhusika duara hubadilika kitabia katika fasihi. Hawana msimamo thabiti. Hubadilika kulingana na maudhui na mazingira. Kwa mfano, msichana aliyeanza kama mpole na mwadilifu anapobadilika na kuwa mtovu wa nidhamu, kahaba na asiyeshirikiana na mtu yeyote.
- Wahusika Wafoili ⇒ huwa katikati ya wahusika bapa na wahusika duara. Wanaweza kuchukua msimamo fulani katika maswala fulani lakini pia wanaweza kubadilisha msimamo huo wakati mwingine kulingana na hali. Wahusika hawa hutegemea wahusika duara na wahusika bapa ili kutoa sifa zao. Kwa mfano, wakiishi na mhusika bapa, wanaweza kuchukua msimamo wa mhusika huyo lakini wakikaa sana na mhusika mwengine, wanabadilika. Wahusika hawa aghalabu huwakilisha uhalisi wa binadamu.
Kuna aina mbili za wahusika bapa:
Comments
Post a Comment